
Na Baraka Mpenja
Leo
hapatoshi uwanja wa taifa majira ya saa kumi kamili jioni ambapo
wawakilishi pekee wa Tanzania michuano ya kimataifa barani Afrika, klabu
ya Azam FC itakuwa na kibarua kizito mbele ya timu ya jeshi la Morroco,
AS FAR Rabat, katika dimba la taifa jijini Dar es salaam.
Azam
FC ina fursa nzuri ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo itakayochezeshwa
na mwamuzi Emile Fred kutoka Shelisheli kutokana na maandalizi
iliyofanya.
Makocha
wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen
Ouadani wa AS FAR Rabat walizungumza jana na waandishi wa habari kuhusu
mechi hiyo, kuwa wamejiandaa kuibuka na ushindi.
Kocha Ongala alisema wamepata DVD za mechi tatu za mwisho za AS FAR
Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al Nasir ya Libya ambayo waliitoa
katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na nyingine mbili za ligi
ya Morocco ambazo wanazifanyia kazi kuhakikisha wanashinda kesho.
Naye
Ouadani alisema hawaifahamu vizuri Azam, lakini wanaujua mpira wa
Tanzania baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya
Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa
jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na Stars kushinda mabao 3-1.
Baadhi
ya wachezaji ambao Azam inatarajia kuwatumia kwenye mechi ya leo ni
pamoja na Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum
Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars kilicho
chini ya kocha Kim Poulsen.
AS
FAR Rabat ina wachezaji sita kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji
hao ni mabeki Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal,
na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.
0 comments:
Post a Comment