PIGO JUU YA PIGO SIMBA SC; SHOMARY KAPOMBE AUMIA BEGA NA HATACHEZA DHIDI YA AZAM FC
PIGO tena Simba SC. Nahodha Msaidizi wa Wekundu wa Msimbazi, Shomary Kapombe ameumia bega na atatakiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki nzima akipata tiba.
Kapombe aliumia bega hilo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, dhidi ya wenyeji Toto African.
Kutokana na kuumia katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2, Kapombe sasa atakuwa nje ya Uwanja Aprili 13, mwaka huu wakati Simba ikimenyana na Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.
Tayari Simba SC inamkosa kiungo Kiggi Makassy aliyeumia goti katika mchezo wa kirafiki dhidi ya CDA mjini Dodoma wiki mbili zilizopita na anatakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji India.
Aidha, Simba imewasimamisha wachezaji wake ‘mafaza’ kadhaa, Juma Nyosso, Haruna Moshi ‘Boban’, Amir Maftah, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Komabil Keita, Abdallah Juma na Paul Ngalema kutokana na utovu wa nidhamu.
Kwa sasa kikosi cha Simba kinaundwa na chipukizi zaidi waliopandishwa kutoka kikosi cha pili, Simba B wakiongezewa nguvu na wakongwe wachache, Nahodha Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amri Kiemba na Mrisho Khalfan Ngassa.
Simba yenye pointi 35 katika nafasi ya nne, ni kama imekwishavuliwa ubingwa wa Ligi Kuu, kutokana na kuachwa mbali na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 49, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 43 na Kagera Sugar pointi 37.
Tayari kikosi cha Simba kipo Dar es Salaam tangu jana jioni kikitokea Kanda ya Ziwa ambako kilicheza mechi za Ligi na za kirafiki. Kesho Simba itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment