By Baraka Mpenja
KUFUATIA mkoa wa Mbeya kuwa mwenyeji wa michuano ya mpira wa pete `netiboli` ngazi ya taifa
septemba mwaka jana, sasa mchezo huo unaonekana kuwa na hamasa kubwa kwa wadau hususani
makampuni mbalimbali ya simu na makampuni
binafsi ya kibiashara.
Katika mashindano
hayo ya kitaifa Shule inayomilikiwa na mwanariadha wa zamani wa Tanzania na
rais wa kamati ya Olympic Tanazania, OT, Filbert Bayi, inayojulikana kwa jina
la “Filbert Bayi School” walitwaa ubingwa,
huku Jeshi stars wakishika nafasi ya pili na JKT Mbweni nafasi ya tatu.
Akizungumza leo na
mtandao huu, mwenyekiti wa chama cha mpira wa pete jijini Mbeya, Mary Mng`ong`o
amesema hali ya mchezo huo uliolala kwa muda mrefu inatia matumaini kufuatia wadau mbalimbali
kuendelea kuchangamkia mchezo huo unaopeperusha vyema bendera ya taifa la
Tanzania.
“Hali imekuwa nzuri
sana, kwa mfano Mei mosi itafanyika kitaifa mkoani Mbeya, kulikuwa na timu
nyingi zilizoomba kushiriki, kutokana na mashindano hayo kuwa ya kitaifa na
kuwa na kiingilio kikubwa tumeamua kuwa na timu chache miongoni mwa timu nyingi
sana zenye nia ya kushindana siku hiyo”. Alisema Mng`ong`o.
Mwenyekiti huyo
aliongeza kuwa kabla ya michuano ya kitaifa kufanyika mkoani humo, mpira wa
pete ulisahaulika kabisa, lakini sasa mwamko umekuwa mkubwa kwa viongozi wa
serikali, vyama na wadau wa michezo ambao kwa pamoja wanaonesha nia ya
kuchangia na kudhamini mashindano ya ndani ya mkoa kwa siku za usoni.
“Unapoona watu
binafsi na makampuni wanaonesha azima ya
kudhamini mpira huu, kama viongozi tunajiridhisha na majibu yetu kuwa, hamasa
inazidi kuwa kubwa na tunaamini baada ya miaka michache ijayo mkoa wetu utakuwa
kitovu cha wachezaji wa netiboli kitaifa”. Alisisitiza Mng`ong`o.
Akizungumzia mikakati
yao kwa sasa, kiongozi huyo anayesifika kuwa mvumilivu wa changamoto za
kiutendaji, alisema ni kuangalia uwezekano wa kuyafikia maeneo yote ya jiji ili
kuhamasisha zaidi mchezo huo.
Mng`ong`o alisema
wana mpango wa kuanzisha mpango maalumu wa kusaka vipaji na kuhamasisha mchezo
huo kuanzia ngazi ya kata, Tarafa na wilaya zote ili kupata timu nzuri na kali
ya mkoa itakayowakilisha mkoa michuano ya kitaifa.
“Ukiangalia maeneo
mengi ya vijijini, kuna vipaji vingi vya wanamichezo,tunalijua hilo, na ndio
maana tunahakikisha tunafungua njia ya kuwafikia wote ili watumie vipaji vyao
kwa faida ya mkoa na taifa”. Alisisitiza Mng`ong`o.
Pia aliwataka wadau kuendelea
kujitokeza kuwachangia ili wafanikishe malengo yao ya kuboresha mchezo huo.
Alisema mwaka jana
wakati wa mashindano walipata shida sana kuendesha mashindano ya kitaifa kutokana
na ukata mkubwa licha ya wadau kuwachangia kiasi kidogo cha fedha.
Mpaka sasa kiongozi
huyo alisema wanadaiwa na watu binafsi ambao chama kiliwapigia magoti ili
kufanikisha mashindano, hivyo mwaka huu wanaomba watu wajitokeze kwa wingi
kuwachangia katika mashindano watakayoanzisha pamoja nay ale ya Mei Mosi.
0 comments:
Post a Comment