Na Baraka Mpenja
Makampuni makubwa yanayojitokeza kudhamini
timu kubwa za ligi kuu soka Tanzania bara yametupiwa lawama kwa kukimbia
majukumu yao ya kuwekeza katika soka la vijana ambalo ndio msingi wa kupanda
kwa kiwango cha mchezo huo nchi yoyote
duniani.
Akizungumzia na mtandao huu kutoka
jijini Mbeya, kocha msaidizi wa klabu mpya ya lgi kuu msimu ujao, Mbeya city na
mkurugenzi wa kituo cha kulea na kuibua vipaji cha “Forest Youth Academy”,
mwalimu Maka Mwalwisye amesema makampuni yangekuwa na nia ya kuendeleza soka yangewekeza katika soka la vijana ili kupata
wachezaji makinda.
“Siku zote nyumba haiwezi kusimama bila
msingi, na huwezi kuvuna mahindi bila kupanda, lazima vijana waandaliwe kwa
juhudi zote, kama makampuni yatajitokeza kusaidia vitua vya soka la vijana
itasaidia zaidi kusonga mbele”. Alisema kocha Mwalwisye.
Kocha huyo alitolea mfano kikosi cha
sasa cha Taifa stars kilichosheheni makinda wengi ambao msingi wao wa kucheza
kandanda umeanzia soka la vijana
husasani michuano ya Copa Coca Cola.
“Watu wanasahau, wakati kocha Kim
Paulsen akikabidhiwa majukumu ya kukinoa kikosi cha Stars alikuwa kocha wa timu
za vijana, alitumia muda mwingi kuwafundisha vijana ambao baadaye aliamaua
kuwatumia timu ya taifa, sasa timu inafanya vizuri, lakini bado makampuni
yanashindwa kujiingiza katika soka la vijana”. Aliongeza Mwalwisye.
Pia alisisitiza kuwa timu ya taifa
imejaza makinda wanaoonesha soka safi, lakini soka linakwenda na wakati, hivyo
kama jitihada za kuwekeza soka la vijana zitasahaulika, basi tutarudi wakati ule
wa kuzomea Taifa stars kwani itakosa wachezaji wengine.
Kocha huyo aliongeza kuwa yeye kama mdau
mkubwa wa soka na mwalimu wa mchezo huo aliamua kuanzisha kituo cha kulea na
kuibua vipaji mwaka 2001 na sasa amaepata mafanikio makubwa sana kufuatia
kuzalisha wachezaji wengi wanaocheza ligi kuu na ligi daraja la kwanza.
“Nimefanikiwa kuwa na kituo changu ingawa
bado ninahitaji msaada mkubwa katika suala la vifaa kama mipira na chezi. Mimi
ni mtaalamu na huwa nashona mwenyewe mipira pale ninaposhindwa kupata vifaa kwa
wakati, hakika kuendesha kituo sio kazi nyepesi kama watu wanavyofikiria”.
Alisema Mwalwisye.
Akipendekeza nini kifanyike, Mwalwisye
amewataka wadau wa michezo na vyombo vya habari kufanya makongamano ya michezo
ili wadau wakutane na kujadili mstakabali wa soka la vijana.
Pia alivitaka vyombo vya habari
kuwaelimisha watu wenye makampuni ili wajiingize kujenga misingi ya soka la
taifa kwa kuwekeza katika soka la vijana ambalo ndio kama msingi wa nyumba.
Mnamo mwaka jana Kocha Maka Mwilwisye alikiongoza
kikosi cha timu ya vijana ya mkoa wa Mbeya katika michuano ya Copa Coca Cola
iliyofanyika jijini Dar es Salaam, lakini alitolewa hatua ya awali ya michuano
hiyo.

0 comments:
Post a Comment