Na Baraka Mpenja
Ligi kuu soka visiwani Zanzibar "Grant Malta" iliyosimama
kwa wiki moja kupisha sherehe za pasaka ,inatarajiwa kuendelea kushika kasi aprili
nne mwaka huu kwa viwanja mbalimbali kuwaka moto.
Akizungumza kwa njia ya simu na
mtandao huu kutoka visiwani Zanzibar, katibu mkuu wa chama cha soka visiwani
Zanzibar, Masud Ettei, amesema patashika la ligi hiyo limetawaliwa na ushindani
mkubwa hususani kwa timu zinazowania taji na zile zinazopambana kukwepa rungu
la kushuka daraja.
Katibu huyo alisema vinara KMKM
wanashindana kufa na kupona na wapinzania wao wa karibu klabu ya Chuoni FC, pamoja
na timu za Mafunzo na Zimamoto, ambazo kwa pamoja zinawania ubingwa msimu huu.
“Ushindani wa timu ni mkubwa sana,
lakini hali ni hatari zaidi kwa timu za Malinzi, wakongwe Zanzibar, Mundu ,Super
Falcon na Duma ambazo zinachuana kukwepa mkasi wa kuporomoka daraja”. Alisema Ettei.
Kuhusu timu kutumia vijana, Ettei
alisema Zanzibar makinda wanacheza sana ligi ya huko, kwani kila timu ina wachezaji
yosso wasiozidi miaka 24 pamoja na wakongwe wachache katika vikosi vyako.
“sisi ZFA mara nyingi tunahimiza soka
la vijana, timu za ligi kuu zinaonekana kuwaamini vijana wadogo na kuwatumia
zaidi, hali hii imepelekea makinda wengi kupata nafasi ya kuonesha vipaji vyao
katika soka la ushindani”. Alisema Ettei.
Pia Ettei aliongeza kuwa mashabiki wa
soka visiwani humo mara zote wanaikubali sana ligi ya huko licha ya kuwepo
changamoto za hapa na pale ambazo ni suala la dunia nzuri.
Akizungumzia mikakati yao, katibu
huyo alisema ZFA inafanya jitihada kubwa kuifanya ligi hiyo iwe na ushindani mkubwa
pamoja na ubora wa kutosha ili kuvutia zaidi wawekezaji katika mchezo wa
kandanda.
Pia alisema wanatambua kuwa soka la
kisasa ni kutumia vijana wadogo wenye uwezo mkubwa na kasi kubwa, hivyo
wanajipanga kupanua wigo zaidi kwa makinda kushiriki mashindano mbalimbali
pamoja na michuano ya ligi kuu ili kupata timu bora ya Taifa.
Zanzibar ni moja kati ya wanachama wa
shirikisho la soka barani Afrika CAF na timu zake huwa zinacheza ligi zake
yaani kombe la shirikisho na ligi ya mabingwa barani Afrika.
0 comments:
Post a Comment