Na Baraka Mpenja, Dar
es Salaam
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya mchezo
wa Tenisi Tanzania, Kiango Kipingu, amewataka wadau wenye nia ya kuendeleza
mchezo huo kujitokeza kuomba nafasi za uongozi ndani ya chama cha Tenisi
Tanzania ili kuinua kiwango cha mchezo huo unaoonekana kushuka sana.
Kipingu amesema kuwa imefika wakati wa kupata viongozi ambao sio
wachumia matumbo yaani wanaojali zaidi maslahi binafsi na kusahau majukumu yao
ya kuendeleza mchezo huo.
“Unajua hali ya Tenisi Tanzania ni
mbaya sana, hakuna watu wenye udhati wa kuinua mchezo huu, hivyo ni muhimu watu
wakajitokeza kuingia katika mchezo wa tenisi ili kufikia mafanikio makubwa zaidi”.
Alisema Kipingu.
Kocha huyo aliyeanza kucheza mchezo
huo miaka 20 iliyopita mjini Morogoro na baadaye 1996 shirikisho la mchezo huo
duniani ITF kumpeleka Afrika kusini kucheza mchezo huo, alisema banafsi
hakupanga kuingia katika kazi ya ukocha, lakini ubabaishaji mkubwa nchini
Tanzania ndio siri ya yeye kujimwaga katika ukocha.
“Nchi yetu iko nyuma sana, hakuna
ubunifu wa mashindano mbalimbali, vijana wanakatishwa tamaa kwa kukosa milango
ya kutokea, hakika nikaamua kuachana na
uchezaji na kuingia katika ukocha”. Aliongeza kipingu.
Kipingu ambaye aliishi kwa muda mrefu
nchini Afrika kusini katika mji wa Pretoria na kucheza mchezo huo kwa
mafanikio, alisisitiza kuwa lengo lake lilikuwa kushiriki michuano ya
Wembleydone, lakini safari imekuwa ndefu na sasa anawaza kulisaidia taifa
kuhamasisha mchezo huo.
Akizungumzia mipango yake, Kipingu
alisema anahitaji kuanzisha kituo chake cha kuibua na kulea vipaji, ingawa bado
ana safari ndefu sana kutokana na kukosekana kwa masaada kutoka kwa wadau na
viongozi wa serikali.
Pia alisema kuwa kwa sasa anaendesha
programu za mchezo huo katika timu tofauti, shule tofauti za msingi, lakini
malipo yake yamekuwa ya kusuasua sana.
Kipingu alisisitiza kuwa yeye ana
uwezo mkubwa sana, lakini kinachomwangusha ni hali ya viongozi kutothamini
makocha wazawa.
“Angalia timu ya vijana ilivyofanya
vizuri hivi karibuni katika mashindano ya kanda ya tano afrika, lakini juzi
juzi wameleta kocha wa kigeni kutoka Msiri, amekula fedha nyingi bila kazi ya
maana, mimi ambaye nafundisha timu mbalimbali akiwemo ya taifa kwa mafaniko
nadharauliwa.”Aliongeza Kipingu.
Kocha huyo mwenye moyo wa kujitolea
alisema ni wakati mwafaka kwa viongozi wa mchezo huo kuweka mikakati maalumu ya
kuendeleza mchezo huo kwa kushirikiana na watu binafsi wenye nia kama yeye.
Pia alisema yeye alizaliwa Kigamboni
jijini Dar es Salaam hivyo anataka kupeleka kituo cha mchezo huo katika
kitongoji chake, na aliwataka watu wengine kuiga mafano huo ili kuyafikia
maeneo mengi ya Tanzania.
0 comments:
Post a Comment