Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Mikikimikiki
ya ligi kuu Vodacom Tanzania bara inatarajia kuendelea jioni ya leo
katika dimba la taifa ambapo waliokuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo,
wekundu wa msimbazi Simba “Taifa kubwa” watawakaribisha wapiga kwata wa
Polisi Morogoro katika dimba la taifa maeneo ya Chang`ombe jijini Dar es
salaam.
Mchezo huo unatarajia kuwa mkali kutokana na umuhimu wa matokeo ya ushindi kwa timu nzote mbili.
Mnyama
Simba ambaye tayari ameshapoteza ubingwa wake na kuwakabidhi watani
zake wa jadi Dar Young Africans “Kwalalumpa Malysia” anahitaji ushindi
kufa na kupona ili kupigania angalau nafasi ya pili na kulinda heshima
yake.
Simba
ambaye msimu huu mambo yamemwendea mrama anatarajia kutumia kikosi
kilekile cha makinda wake ambao wanawajenga kwa ajili ya msimu ujao, pia
kujiandaa kukumbana na Yanga mechi ya funga pazia ya ligi kuu msimu wa
2012/2013 uwanja wa taifa mwezi mei mwaka huu.
Akiongea na MICHEZO BOMBA!
Kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kiwhelu “Julio Alberto” aliseama leo
hii mchana wamekaa kikao na wachezaji wao ili kuwapa morali na kuwaeleza
umuhimu wa kushinda katika mchezo wa leo.
“Ninavyokuambia
hivi tupo katika kikao cha pamoja na wachezaji wetu, tunaelezana
machache kabla ya kwenda uwanja wa taifa kuvaana na polisi Morogoro,
maandalizi yetu ni mazuri na tuna imani ya kushinda”. Alisema Julio.
Julio
aliongeza kuwa mashabiki na wanachama wa wekundu wa smimbazi Simba
lazima watambue kuwa timu yao ipo wakati wa mpito, kinachotakiwa kwa wao
ni kuwaunga mkono vijana wao ambao wanajengwa kuleta matunda msimu ujao
wa ligi.
“Leo
hii watu wanaiona Simba haina lolote, sisi tunasema hiki kikosi ambacho
kinaandaliwa na benchi la ufundi kitakuwa moto wa kuotea mbali sana, na
siku zote tunamshukuru Mungu kwa kutupa uzima na tuna matarajio makubwa
sana na vijana wetu”. Alisema Julio.
Wakati
Mnyama akijinasibu kushinda mchezo wa leo, nao Polisi Morogoro walisema
maandalizi waliyoyafanya yanatosha kupata ushindi mbele ya Simba.
Afisa habari wa klabu hiyo, Clememce Banzo ameiambia MICHEZO BOMBA! kuwa endapo watapoteza mchezo wa leo watazidi kujichimbia kaburi wenyewe na kujizika ndani yake.
“Maji
yameshafika shingoni, hakika hatuna hali mpaka sasa na tukifungwa na
Simba, safari ya kutoa mkono wa bai bai kwa ligi kuu ya Tanzania bara
itakuwa imeshafika”. Alisema Banzo akiwa amekata tamaa.
Banzo
aliongeza kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Rishard Adolf tayari amehawapa
mazoezi mazuri na kuwapanga kisaikolojia wachezaji wake kupambana na
simba leo hii.
Siku
zote soka ni dakika tisini, aliyejipanga na kuwa na nidhamu ya mpira
dimbani anaweza kupata ushindi, leo Simba ama Polisi yoyote anaweza
kutwaa pointi tatu muhimu, dakika za mwamuzi zinasubiriwa.
0 comments:
Post a Comment