Kocha wa Azam FC, Stewart Hall akizungumza na Florian Kaijage Mratibu wa klabu katika mashindano ya Afrika, baada ya kuwasili Cassablanca leo |
Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
AZAM FC imewasili salama nchinio Morocco tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji, FAR Rabat, Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi wiki hii.
Azam, imewasili Cassablanca, majira ya saa 9:15 za huku Alasiri, sawa na saa 10:15 za Afrika Mashariki na kusafiri kwa basi kwa saa mbili kwenda Rabat, mji ambao mechi itachezwa.
Azam imetua Morocco ikitokea Dubai, UAE ambako ilifika usiku jana saa 6:00 kwa saa za huko sawa na saa 5:00 kwa saa za Afrika Mashariki, ikitokea Dar es Salaam.
Msafara huo unaouhusisha wachezaji na benchi la Ufundi, baada ya awali viongozi na wapenzi kadhaa kutangulia nchini humo, ili kuweka mazingira sawa, uliondoka Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la Emirates, wadhamini wa Arsenal ya England saa 11:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Ni safari ndefu iliyohusisha mabara mawili, kutoka Afrika, Tanzania kupitia Asia Dubai na kurudi Afrika nchini Morocco.
Azam walilala katika hoteli ya nyota tano ya Copthorne Dubai kabla ya kuunganisha ndege saa 7:35 asubuhi ya leo kuja Morocco kesho.
Wachezaji wanawasili Morocco |
Azam imefikia katika hoteli ya Golden Tulip, maeneo ya Rabat, kaskazini mwa Cassablanca, kilomita 120 kutoka Uwanja wa Ndege wa Cassablanca, umbali wa takriban saaa mbili.
Azam itaanza rasmi mazoezi kesho kujiandaa na mchezo huo, ambao wanatakiwa kutoa sare ya mabao au kushinda ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Japokuwa hilo linachukuliwa kama jambo gumu mbele ya wengi, lakini rekodi ya timu hiyo, mali ya bilionea Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inaonyesha linawezekana.
Wachezaji wanatua Morocco |
Azam imekuwa ikicheza vizuri na kupata matokeo mazuri katika mechi za ugenini kwenye michuano hii, kuliko nyumbani na hata kufuzu kwake hadi hatua hii zaidi kulitokana na matokeo ya mechi za ugenini.
Raundi ya kwanza, Azam ilianza kwa kushinda kwa taabu 3-1 Dar es Salaam dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini, sehemu kubwa ya mchezo huo matokeo yakiwa 1-1 kabla ya mabao ya dakika za jioni ya Kipre Tchetche kutengeneza ushindi huo.
Mchezo wa marudiano, Azam ilishinda 5-0 ugenini na kufanya ushindi wa jumla wa 8-1, ikisonga mbele kibabe.
Raundi ya Pili, ilianza kwa ushindi wa 2-1 ugenini, Liberia dhidi ya wenyeji, Barack Young Controllers II, lakini katika mchezo wa marudiano ilibanwa kwa sare ya 0-0.
Kocha Muingereza Stewart Hall hakuipa umuhimu mechi ya Ligi Kuu Ijumaa dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga iliyoisha kwa sare ya 1-1 akiwapumzisha wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi na FAR Rabat.
Wakati mabeki Waziri Salum, Joackins Atudo, viungo Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Balou na mshambuliaji Kipre Tchetche hawakukanyaga kabisa nyasi za Uwanja wa Mkwakwani Ijumaa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alicheza kwa dakika 15 tu za mwisho- ili kuhakikisha wanakuwa vizuri Jumapili mjini Rabat.
Kutoka kikosi cha kwanza cha sasa cha Azam waliocheza dakika zote juzi ni kipa Mwadini Ally, kiungo aliyehamishiwa beki ya kulia, Himid Mao, beki David Mwantika, kiungo Humphrey Mieno na washambuliaji Brian Umony na John Bocco ‘Adebayor’.
Azam, itakuwa Rabat kwa wiki nzima hadi Jumamosi itakapocheza mechi na imejipanga vema kuhakikisha inavuka hatua hii.
0 comments:
Post a Comment