Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Hamisi Kiiza (wa tatu kutoka kulia) baada ya kufunga bao pekee leo |
BAO pekee la Hamisi Kiiza ‘Diego’ jioni ya leo limezidi kuisogeza Yanga SC karibu na ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuilaza 1-0 Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifga, Dar es Salaam.
Yanga sasa ina pointi 48 baada ya kucheza mechi 21, ikiizidi kwa pointi 11 Azam FC iliyo katika nafasi ya pili, ingawa ina mchezo mmoja mkononi.
Simba SC inaendelea kushika nafasi ya tatu kwa pointi zake 34.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Jacob Adongo kutoka Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu wa Mbeya, hadi mapumziko milango ilikuwa migumu.
Yanga walicheza vizuri kama kawaida yao, lakini walikosa mipango ya kumalizia mashambulizi yao.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Errnie Brandts leo aliwaanzisha Nizar Khalfan na Hamisi Kiiza katika safu ya ushambuliaji, akiwaweka benchi washambuliaji tegemeo wa timu hiyo Didier Kavumbangu, Jerry Tegete na Said Bahanuzi.
Nizar Khalfan alikosa bao la wazi dakika ya tano, baada ya kutegua vizuri mtego wa kuotea wa mabeki wa Ruvu, lakini pamoja na kujisogeza karibu na kipa Benja Haule ili amfunge vizuri, ajabu alipiga nje.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi nzuri zaidi kwa Yanga kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili Yanga SC walikianza kwa kasi tena na iliwachukua dakika tatu tu kujihakikishia ushindi katika mchezo wa leo.
Ilikuwa ni kazi nzuri ya kiungo Frank Domayo ambaye baada ya kuwatoka wachezaji wa Ruvu, alimpasia Nizar aliyemtengea mfungaji, Kiiza ambaye bila ya ajizi akawianua vitini mashabiki wa Yanga.
Baada ya bao hilo, Yanga iliendelea kushambulia langoni mwa Ruvu, lakini kutokana na kutokuwa na mipango mizuri ya kumalizia mashambulizi yao, hawakuweza kupata bao la kuongeza.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua/David Luhende dk45, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Hamisi Kiiza, Nizar Khalfan/Didier Kavumbangu dk80 na Haruna Niyonzima.
Ruvu Shooting; Benja Haule, Michael Aidan, Mau Bofu, Ibrahim Shaaban, Mangasini Mbonosi, Gedion Tepo/Paul Ndauka dk56, Ayoub Kitala/Raphael Kyala dk83, Ernest Ernest, Hassan Dilunga, Said Dilunga na Abrahman Mussa/Kulwa Mobi dk57.
0 comments:
Post a Comment