Na Boniface Wambura, Tff
>>VPL: LYON KUJUA MUSTAKABALI WAKE CHAMAZI
LYON KUJUA MUSTAKABALI WAKE CHAMAZI
HATMA ya African Lyon kuendelea kushika
mkia au la kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inajulikana leo wakati
itakapokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam.
Lyon yenye pointi 13 kutokana na mechi
19 inabidi iifunge Ruvu Shooting kama inataka kuirejesha mkiani Toto
African yenye pointi 14. Kama kweli inazitaka pointi zote tatu itabidi
ifanye kazi mbele ya Ruvu Shooting inayotiwa makali na Kocha Charles
Boniface Mkwasa.
Hiyo itakuwa mechi ya 18 kwa Ruvu
Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26 ikitanguliwa na
vinara wa ligi hiyo Yanga, Azam, Simba, Coastal Union, Kagera Sugar na
Mtibwa Sugar yenye pointi 28 ikinolewa na nahodha wa zamani wa Taifa
Stars, Mecky Maxime.
Mechi hiyo namba 139 itachezeshwa na
mwamuzi Amon Paul kutoka Musoma wakati wasaidizi ni Anold Bugado wa
Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya. Mwamuzi wa mezani atakuwa
Shafii Mohamed wa Dar es Salaam.
Nayo Tanzania Prisons ya Jumanne Chale
itakuwa mgeni wa Oljoro JKT katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sheikh
Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati Mgambo Shooting itaoneshana kazi
na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kesho (Machi 7 mwaka huu) Uwanja wa
Azam Complex jijini Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya JKT
Ruvu ya Kocha Charles Kilinda na Kagera Sugar.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi ya
Machi 9 mwaka huu kwa mechi mbili; Yanga vs Toto Africans (Uwanja wa
Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).
TFF YAWASILISHA RASMI MAOMBI KUMUONA WAZIRI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limewasilisha rasmi maombi ya kuonana na Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ili kuzungumzia uamuzi wake
wa kutengua usajili wa Katiba ya 2012.
Maombi hayo yaliwasilishwa rasmi
Wizarani hivi karibuni ambapo TFF imependekeza kikao hicho
kifanyike keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) au Machi 13 mwaka huu.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana
Machi 2 mwaka huu kujadili tamko ya Waziri kutengua matumizi ya Katiba
ya 2012 ndiyo iliyopendekeza kikao hicho kwa lengo la kusikiliza upande
wa TFF katika suala hilo.
0 comments:
Post a Comment