BONIFACE WAMBURA MGOYO, MSEMAJI WA TFF |
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeondoa utaratibu wa wadau wake
kuingia bure kwenye mechi kwa kutumia tiketi maalum (free pass).
Kutokana
na uamuzi huo hakutakuwa tena na pasi za bure kwa ajili ya kushuhudia
mechi zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa TFF katika viwanja
mbalimbali nchini.
Uamuzi
huo umetokana na ukweli kuwa free pass zimekuwa zikipunguza au kuchukua
mgawo wote wa TFF kwenye mechi, na wakati mwingine Shirikisho
hulazimika kutoa fedha za ziada kugharamia pasi hizo.
Pasi
zote ambazo imekuwa ikitoa kwa wadau wake hukatwa katika mgawo wa TFF
katika mechi husika. Shirikisho hivi sasa linapata asilimia nne tu ya
mapato katika mechi za Ligi Kuu, ligi ambayo hivi sasa inaendeshwa na
Kamati yake ya Ligi.
RUVU SHOOTING KUIKABILI YANGA VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho
(Machi 16 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu
Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi
Jacob Adongo kutoka Musoma mkoani Mara ndiye aliyepewa jukumu la
kuchezesha mechi hiyo namba 146. Adongo atasaidiwa na Anold Bugado wa
Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya wakati mwamuzi wa mezani ni
Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
Mtathmini
wa waamuzi ni Army Sentimea wakati Kamishna wa mechi hiyo
inayokutanisha vinara Yanga na Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba
ikiwa na pointi 29 chini ya ukufunzi wa Charles Boniface Mkwasa na
Msaidizi wake Selemani Mtungwe ni Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya.
Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh.
8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na B
wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
Pia
TFF inawaasa washabiki wa mpira wa miguu kuacha kununua tiketi mikononi
mwa watu kwa vile wanaweza kuuziwa tiketi bandia. Tiketi zote zitauzwa
katika vituo vinavyotangazwa katika magari maalumu, na uwanjani pia
katika magari hayo.
Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua washabiki 25,000
utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na Mgambo Shooting
kutoka Tanga. Ugumu wa mechi hiyo unatokana na ukweli kuwa timu zote
mbili zinapigana kuepuka kurudi zilikotoka (daraja la kwanza).
Mgambo
Shooting inayonolewa na Mohamed Kampira inashika nafasi ya tisa ikiwa
na pointi 24 katika ligi hiyo yenye timu 14. Toto Africans ambayo iko
nyumbani itaingia uwanjani ikiwa na pointi 14 katika nafasi ya 15 kwenye
msimamo wa ligi.
Baada
ya kulala 2-1 mbele ya Simba katika mechi iliyopita, Coastal Union
itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa
Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
Ligi
hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) kwa mechi moja
itakayozikutanisha JKT Ruvu na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam
Complex.
RAMBIRAMBI MSIBA WA OFISA HABARI CECAFA
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha aliyekuwa Ofisa Habari wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Finny Muyeshi kilichotokea juzi
(Machi 13 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya baada ya kuugua kwa muda
mrefu.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Muyeshi aliitumikia
CECAFA kwa muda mrefu, hasa katika kuhakikisha waandishi wa habari
wanapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi wakati wanaporipoti matukio
mbalimbali ya Baraza hilo.
Alitoa
mchango mkubwa katika eneo la habari za mpira wa miguu, tangu akiwa
gazeti la East African Standard la Kenya akiwa mwandishi, na baadaye
Mhariri wa Michezo kabla ya kujiunga na CECAFA, hivyo mchango wake
tutaukumbuka daima.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Muyeshi, CECAFA, Shirikisho la
Mpira wa Miguu Kenya (FKF) na tasnia ya habari kwa ujumla, na kuwataka
kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo
mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Muyeshi mahali pema peponi. Amina
FDL KUKAMILISHA MSIMU WIKIENDI
Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 unamalizika wikiendi hii huku
timu za Mbeya City ya Mbeya, Ashanti United ya Dar es Salaam na Rhino
Rangers ya Tabora zikiwa tayari zimepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) msimu ujao.
Kundi
A mechi zote zitachezwa Jumapili (Machi 17 mwaka huu) ambapo Majimaji
vs Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Kurugenzi vs
Mkamba Rangers (Mafinga) na Burkina Faso vs JKT Mlale (Jamhuri,
Morogoro).
Kesho
(Machi 16 mwaka huu) katika kundi B itakuwa Green Warriors vs Polisi
Dar (Karume, Dar es Salaam) na Ndanda vs Villa Squad (Nangwanda Sijaona,
Mtwara). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Moro United vs Ashanti
United (Karume, Dar es Salaam) na Tranist Camp vs Tessema (Mabatini,
Mlandizi).
Kundi
C ni kesho (Machi 16 mwaka huu) Polisi Tabora vs Pamba (Ali Hassan
Mwinyi, Tabora). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Polisi Mara vs JKT
Kanembwa (Karume, Musoma), Polisi Dodoma vs Mwadui (Jamhuri, Dodoma) na
Rhino Rangers vs Morani (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
KILA LA KHERI AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam
kwenye mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Barrack Y.C. II
itakayochezwa Jumapili (Machi 17 mwaka huu) nchini Liberia.
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itachezwa jijini Monravia na timu
hizo kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam. Ofisa Habari wa
Azam yuko na timu hiyo Monrovia na anapatikana kwa namba +231888386655.
0 comments:
Post a Comment