Wachezaji wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na Zanzibar
wenye umri kati ya miaka 18 na 21 wametakiwa kuchangamkia fursa ya kufanya
majaribio ya kucheza soka la kulipwa Barani Ulaya, Asia na Afrika wakiwa
nyumbani Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya
Tanzania Mwandi, Teonas Aswile, waandaaji wa Michuano ya African Youth Football
Tournament amesema kuwa katika michuano hiyo wachezaji 11 bora watatafutiwa
timu moja kwa moja katika mataifa nane barani Ulaya (Ufaransa, Ureno, Uholanzi,
Denmark, Norway, Sweden, Ubelgiji na Switzerland), Asia na Afrika.
TEONAS ASWILE Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Mwandi, |
Bwana Teonas Aswile amesema kuwa wachezaji wa Tanzania bado
hawajaonesha muamko mkubwa licha ya kiwango cha chini cha kushiriki ambacho
wamewekewa ikilinganishwa na wachezaji wa kigeni, ambao licha ya kuwekewa USD
500 bado wamezidi kumiminika.
“Mpaka sasa kuna mawakala wawili ambao tumezungumza nao na wamethibitisha
kuleta wachezaji wao zaidi ya 20 kushiriki kwenye michuano.”
“Hii ni mbali ya wachezaji mmoja mmoja ambao tunaowasiliana
nao ambao wanataka kuja, wakiwa zaidi ya watano. Kwahiyo wachezaji wetu waamke
na kuitumia fursa hii ambayo haipo katika nchi nyingine ya Afrika kwa wachezaji
kufanya majaribio nchini mwao.”
Aidha Aswile ameviomba vilabu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwalipia
wachezaji wake ada ya shilingi laki tatu (Tsh 300, 000) ambayo inahitajika kwa
mchezaji ili aweze kushiriki kwenye michuano ya African Youth Football
Tournament kufanya hivyo kwani mchezaji huyo atakapouzwa klabu husika ndiyo
itakayokubaliana na klabu itakayomchukua na si Kampuni ya Tanzania Mwandi.
“Sisi tunachokifanya ni kumuwezesha mchezaji aone njia za
kufikia malengo yake. Kwa hiyo akishafanikiwa na amepata timu ya kuchezea iwe
Ulaya, Asia au Afrika, klabu yake ndio itakayokubaliana na timu ya huko sisi
hatutachukua chochote”, Teonas alisema.
Mkurugenzi huyo akitaja idadi ya wachezaji wa Tanzania ambao
tayari wamethibitisha kushiriki amesema kuwa ni wachezaji watatu jambo ambalo
bado linaonyesha mwamko umekuwa mdogo.
Michuano ya African Youth Football Tournament itafanyika
Tanzania katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 10 hadi 14
mwezi wa sita mwaka huu na kuwashirikisha wachezaji wenye umri wa miaka 18 hadi
21 ambapo watafundishwa na makocha watatu kutoka nje ya nchi na wawili wa
Tanzania.
Pia michuano hiyo itashirikisha mawakala kutoka nchi nane za
barani Ulaya, Asia na Afrika ambao wanahitaji wachezaji kwaajili ya klabu
wanazoziwakilisha kati yao wakiwa ni Budak Johan, Cabrera Oliver, Dag Larsson,
Phillip Mwakikosa na Dahlin Martin huku wakala wa kimataifa wa Tanzania Dr
Damas Ndumbaro akiwa miongoni mwa mawakala wa Tanzania watakaoshiriki katika
michuano kusaka vipaji kwaajili ya klabu mbalimbali.
“Tuna maombi ya mawakala wawili ambao wanataka wachezaji
mabeki, washambuliaji na viungo kwaajili ya klabu zao Kuwait, Qatar, Libya na
sehemu nyingine kwa hiyo hii ndio fursa ya wachezaji wetu kwenda kucheza soka
la kulipwa na lenye maslahi zaidi kwao.”
Imetolewa na Idara ya Habari
Kampuni ya Tanzania Mwandi,
TANCOT House, Ground Floor,
S. L. P 79944,
Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment