MECHI YA TAIFA STARS YAINGIZA MIL 226/-
Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na
Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jana (Machi 24 mwaka huu) na
Stars kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 226,546,000.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi
kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh.
10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo
sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh.
8,625,641.88.
Nyingine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia
15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh.
25,222,854.67 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) sh. 6,305,713.67.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh.
71,885,135.82 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
TENGA AWAPONGEZA WACHEZAJI, SERIKALI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
ameipongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi,
washabiki, mdhamini na Serikali kwa kufanikisha ushindi wa jana.
Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau
wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na
mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.
Amesema Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu,
usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha
kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo ambapo Taifa Stars iliifunga
Morocco mabao 3-1.
MKUTANO WA DHARURA SIMBA SI HALALI
Mkutano Mkuu wa Dharura ulioitishwa na wanachama wa Simba, Machi 17
mwaka huu na kuuondoa uongozi wa klabu hiyo si halali kwa vile
haukufuata taratibu, na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
halitambui Kamati za Muda.
Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
jana (Machi 24 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti
wake Alex Mgongolwa.
Kamati imebaini kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 22(2) ya Katiba ya Simba,
Mkutano Mkuu wa Dharura unaitishwa na Kamati ya Utendaji baada ya
wanachama wasiopungua 500 kuwasilisha ombi hilo kwa maandishi na
kujiorodhesha. Mkutano huo haukuitishwa na Kamati ya Utendaji ya
Simba.
Utaratibu huo haukufuatwa ambapo barua ya Mkutano huo iliandikwa kwa
Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo badala ya Kamati ya Utendaji ya
Simba ambayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Simba.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji ndiyo inayoitisha
Mkutano Mkuu wa Dharura baada ya kuhakiki uhai na uhalali wa wanachama
waliojiorodhesha kuomba mkutano huo.
Kamati imesisitiza kuwa Katiba za wanachama wote wa TFF hazina
kipengele cha kura ya kutokuwa na imani na uongozi (vote of no
confidence), ndiyo maana uko nyuma wanachama wa Yanga, Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Tabora (TAREFA) walipiga kura hiyo, na TFF kutotambua uamuzi wao.
Hata Katiba ya Simba haitoi mamlaka kwa Mkutano Mkuu wa Dharura
kufukuza uongozi uliochaguliwa.
Katiba za wanachama wote wa TFF zimezingatia katiba mfano za
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambazo zinasema
kiongozi ataingia madarakani kwa uchaguzi, na si kuteuliwa (Kamati ya
Muda).
Pia Kamati imesema endapo wanachama wa Simba wangefuata taratibu na
uongozi ukakataa kuitisha mkutano, wanachama wangetuma ombi hilo TFF
kupitia Kamati ya Sheria ili kutoa mwongozo kwa uongozi wa Simba .
TFF ina mamlaka ya kutoa adhabu kwa viongozi wa wanachama wake
wanaokwenda kinyume cha Katiba zao. Pia Kamati imesisitiza kwa
wanachama wa TFF kuitisha mikutano yao kwa mujibu wa taratibu na
Katiba zao, na wale ambao muda umefika wafanye hivyo haraka.
TENGA KUFUNGUA SEMINA ELEKEZI COPA COCA COLA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina elekezi ya michuano ya
Copa Coca Cola itakayofanyika kesho (Machi 26 mwaka huu).
Semina hiyo inayoshirikisha makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu
mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na itafunguliwa na Rais Tenga kuanzia saa 3 kamili asubuhi.
Washiriki wengine katika semina hiyo itakayokuwa na watoa mada kutoka
TFF na wadhamini kampuni ya Coca Cola ni waratibu wa michuano ya Umoja
wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Home
»
»Unlabelled
» TAARIFA KUTOKA TFF LEO
Monday, March 25, 2013
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment