SERIKALI YARIDHIA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF
Jumatano, 20 Machi 2013 16:17
>> RAIS TENGA AIPONGEZA AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO
>>MSAFARA WA MOROCCO KUTUA NCHINI IJUMAA
PATA TAARIFA KAMILI:
Release No. 051
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 20, 2013
SERIKALI YARIDHIA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF
Serikali imekubali mchakato wa uchaguzi
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uendelee kwa sharti la
kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea waliofika mbele ya Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo
mchana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema uamuzi huo umefikiwa kwenye
kikao kati ya uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
chini ya Waziri Dk. Fenella Mukangara, TFF na Baraza la Michezo la Taifa
(BMT).
Amesema baada ya maafikiano hayo, TFF
italiandikia barua Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
ambalo ndilo lililosimamisha mchakato huo ili litume ujumbe wake kwa
ajili ya kusikiliza malalamiko ya wagombea walioenguliwa.
Rais Tenga ambaye ameishukuru Serikali
kwa kuruhusu mchakato huo uendelee, pia ameahidi kuwa uchaguzi wa TFF
utafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali,
na kuwa haki si tu itatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali imetuelekeza uchaguzi ufanyike
kabla ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko ni mbali. FIFA wakija hata
kesho wakituambia endeleeni sisi tuko tayari. Hesabu zetu ziko tayari,
makabrasha yote yako tayari yanasubiri mkutano tu. Labda itakuwa kutoa
muda tu kwa wajumbe walioko mbali waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi
kuwaita ghafla,” amesema.
Amesisitiza kuwa TFF ilishapanga tarehe
ya uchaguzi, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya
walioenguliwa kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki uchaguzi
kwa sababu wanataka kuendelea kubaki madarakani haya maana hata kidogo.
Hivyo amewataka wagombea wote waliofika
kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wakaendelea kujiandaa vizuri,
kwani FIFA watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
Pia amesema TFF ina heshimu Serikali na
itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima iheshimu FIFA sababu
iko kwenye mpira wa miguu, na FIFA ndiyo wasimamizi wa mchezo huo
duniani.
Amewakumbusha wanachama wa TFF, hasa
wajumbe wa Mkutano Mkuu kufahamu kuwa TFF ina katiba, lakini ni lazima
pia wafahamu kwanini kuna FIFA.
Rais Tenga amewahadharisha watu
wanaopitapita mikoani kuomba saini za wajumbe ili kuita Mkutano Mkuu wa
dharura wakati wanajua mkutano ulishaitishwa, lakini ukasimamishwa na
FIFA. Jambo hilo kikatiba ni kosa.
RAIS TENGA AIPONGEZA AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameipongeza klabu ya Azam kwa ushindi wa
mabao 2-1 ilioupata timu yake katika mechi ya raundi ya kwanza ya
michuano ya Kombe la Shirikisho.
Mechi hiyo dhidi ya Barrack Young
Controllers II ilichezwa jijini Monrovia, matokeo ambayo yanaweka Azam
katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya mchezo wa marudiano
utakaofanyika wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Amesema Azam imefanya jambo kubwa, kwani
kushinda ugenini hasa katika nchi za Afrika Magharibi si jambo dogo,
hivyo Watanzania waendelee kuiunga mkono na anaitakia kila la kheri
katika mashindano hayo.
MSAFARA WA MOROCCO KUTUA NCHINI IJUMAA
Timu ya Taifa ya Morocco (Lions of the
Atlas) inatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa Ijumaa kwa ndege ya
Emirates tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania
(Taifa Stars) itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Msafara wa timu hiyo yenye watu 58
wakiwemo maofisa 19 na waandishi wa habari 12 utawasili Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.55 mchana na utafikia hoteli
ya Kilimanjaro Hyatt Regency.
Siku hiyo Morocco inatarajia kufanya
mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, na Jumamosi
itafanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya
mechi hiyo itakayochezwa saa 9 kamili alasiri.
Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho
chini ya Kocha Rachid Taoussi ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine
Bounou, Younnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir,
Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich na Abdeljalil Jbira.
Issam El Adou, Kamel Chafni, Salaheddine
Saidi, Mohamed Ali Bamaamar, Abdelaziz Barrada, Salaheddine Aqqal,
Abdessamad El Moubarky, Nordin Amrabat, Chahir Belghazouani, Abdelilah
Hafidi, Youssef Kaddioui, Brahim El Bahri, Hamza Abourazzouk na Youssef
El Arabi.
Wakati huo huo, tiketi kwa ajili ya
mechi hiyo zitaanza kuuzwa keshokutwa katika vituo vya Shule ya
Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni
Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa
wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Uwanja wa
Taifa na Dar Live Mbagala.
Milango siku ya mechi kwa ajili ya watazamaji itafunguliwa saa 6 kamili mchana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment