MBEYA CITY |
Na Baraka Mpenja
Kocha mkuu wa klabu mpya ya ligi kuu msimu ujao, Mbeya city ya jijini Mbeya, Mtaalamu Juma Mwambusi, amesema anajiandaa kuwasilisha ripoti yake ya ligi daraja la kwanza aprili 15 mwaka huu katika kikao cha kamati ya utendaji ambacho kitahudhuriwa na viongozi wa serikali ya jiji, viongozi wa timu na kamati ya benchi la ufundi la klabu hiyo.
Kocha huyo anayesifika mwenye kutimiza msemo wa "Hata Mbuyu ulianza kama Mchicha" kwa maana ya kuanza na timu ikiwa kiwango cha chini na hatimaye kuifikisha mbali amesema kuwa ni jambo la kumshukuru mungu kwa kumwezesha yeye na msaidizi wake Mnyakyusa Maka Mwalwisye kuipandisha timu hiyo michuano mikubwa ya ligi kuu soka Tanzana bara masimu wa 2013/2014 huku akicheza soka la kuvutia.
"Binafsi nilizoea kufundisha timu za ligi kuu, baada ya kuingia ligi daraja la kwanza, hali ni hatari, timu zinasakata kandanda la kuvutia, nimejifunza mengi na nitayafanyia kazi kabla ya kuanza ligi mpya, nitawasilisha mapendekezo yangu na nitaanza kupanga kikosi cha vita" alisema Mwambusi.
MWAMBUSI AKIWASHUKURU WANAMBEYA KWA KUWASAPOTI KATIKA SAFARI YAO |
Mwambusi alisema katika kikao hicho anatarajia kuwasilisha ripoti yake itakayohusisha changamoto walizokumbana nazo ligi daraja la kwanza, hali ya kikosi chake na mapendekezo ya maeneo ya kufanyia marekebisho kabla ya kuanza mitanange ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Akiongea kwa kujiamini, Mwambusi alitamba kutumia falsafa yake ya kutumia vijana chipkizi katika ligi ambayo inahusisha timu vigogo kama wekundu wa msimbazi Simba, wazee wa Uturuki Yanga, wana lambalamba Azam fc ,wana tamutamu wa Mtibwar na wana ngulukumbi wa kaitaba, kagera sugar.
"Kwa mtu aliyeiona timu yangu, imechanganya damu changa na kongwe, msimu wa ligi nitawapika vijana wadogo, lakini pia nitasajili wakongwe kadhaa ili kuwepo na ushindani mkubwa ndani ya kikosi changu cha vita". aliongeza Mwambusi.
Kocha huyo aliyewahi kuwafundisha maafande wa jeshi la magereza, Tanzania Prisons " wajela jela" na kuwafikisha mbali alisema makali ambayo Prisons walikuwa nayo wakati akiwa na timu hiyo, sasa yamerejea kwa Mbeya city, hivyo timu za ligi kuu zijiandae kupambana naye kwa mara nyingine.
Pia Mwambusi aliwataka wapenzi wa soka jijini Mbeya kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao ya nyumbani kwani ana mikakati mikubwa ya kuifanya iwe timu kali zaidi katika soka la bongo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha soka jijini Mbeya, MREFA, Elias Mwanjala amesema wananchi wa jiji la Mbeya wanahitaji kutambua kuwa timu za Mbeya city na Prisons ni timu zao na wanatakiwa kuwa karibu nazo kwa kudumisha uzalendo.
Mwanjala alisema katika kikao cha kamati ya utendaji mwezi aprili mwaka huu, watajadili mstakabali wa soka jijini Mbeya sambamba na kupitia ripoti ya mwalimu Mwambusi ili kuweka mikakati ya pamoja kuwasaidia wakali hao wa jiji.
"Hesabu zetu kwa sasa ni kuhakikisha Prisons inasalia ligi kuu ili tuwe na timu mbili,lakini tuna mipango ya kufa na kupona tukishirikiana na wadau ili kuurudisha mkoa wetu katika soka la ushindani kama miaka ya nyuma". Alisema Mwanjala kwa kujiamini.
Naye aliyekuwa mwenyekiti wa MREFA na kumrithisha mikoba ya utawala mwenyekiti wa sasa, mzee John Mwamwaja "Mnyambala" amewataka viongozi wa chama na timu kushirikiana sana ili kufikia malengo yao ya pamoja.
Mwamwaja alisema miaka ya nyuma watu wa Mbeya walishirikiana sana na viongozi wao ili kuifikisha mbali Tukuyu stars "Banyambala" na hatimaye walitisha nchini Tanzania na kutwaa ubingwa wa ligi kuu.
Mbeya ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania iliyosifika sana kuwana timu nzuri na wachezaji wazuri waliotamba na timu za Tkuyu stars, Meko na Sigara
0 comments:
Post a Comment