Na
Baraka Mpenja
Kwa
msaada wa mtandao
“Havumi lakini yumo”, Mashabiki wengi wa soka duniani ni
mara chache sana kulitaja jina la Bastian Schweinsteiger wa Bayern Munich na
timu ya taifa ya Ujerumani kama mchezaji bora zaidi duniani kama ilivyo kwa
akina Lionel Andrew George Messi wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina
pamoja na Cristiano Ronaldo wa Real Mdrid na timu ya taifa ya Ureno.
Kama unajua mpira, miongoni mwa wachezaji wenye kipaji cha
ajabu katika mchezo wa soka duniani, huwezi kumwacha Schweinsteiger wa Bayern
kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga, kumiliki mpira, kupiga pasi
sahihi, kufunga mabao na kuzuia hatari langoni mwake.
Makala hii imejaribu kumchambua nyota huyu kwa kuangalia historia
yake, mafanikio machache kati ya mengi aliyoyapata katika mchezo wa soka akiwa
na Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani pamoja na maisha yake nje ya
soka yakiwemo mapenzi ambayo ni gumzo dunia nzima
Schweinsteiger alianza kucheza kama
winga na baada ya mchezaji Louis van
Gaal kujiunga na Bayern, nyota huyo alianza kupiga dimba la
kati akiwasaidia washambuliaji Arjen Robben
na Franck Ribéry.
Sifa na uwezo wa nyota huyu zinamfanya kuwa mchezaji mkali katika soka la
ujerumani na kuwa miongpni mwa nguzo imara ya klabu ya Bayern Munich pamoja na
timu ya taifa ya Ujerumani.
Nyota huyo amekuwa akiitwa na kocha wa
timu ya taifa ya ujerumani, Joachim Low kuwa ni ubongo wa timu ya taifa ya
Ujerumani kutokana na uwezo wake mkubwa alionao kutawala dimba na kuichezesha
timu.
Schweinsteiger
alizaliwa Agost mosi 1984 katika mji wa kolbermoor magharibi mwa Ujerumani. An
urefu wa futi 6 na anacheza nafasi ya kiungo wa kati katika klabu ya Bayern
Munich maarufu kama “The Barvarian”.
Safari ya soka la kijana huyu kivutio kwa wapenda michezo
nchini Ujerumani iliianza kuwaka mnamo mwaka 1990.
Mwaka 1990-1992 aliichezea klabu ya FV Oberaudorf, 1992-1998
alijiunga na TSV 1860 Rosenheim na 1998-2002 alijiunga na wakali wa Bundesliga Bayern
munich.
2002-2004 alicheza kikosi cha pili cha Bayern na ndani ya
miaka hiyo hiyo miwili aliingizwa kikosi cha kwanza cha Bayern Munich kutokana
na uwezo mkubwa aliounesha.
Kwa upande wa timu ya taifa, 2004 alichezea kikosi cha Ujeruamani
chini ya miaka 21 na 2004 hiyo hiyo aliitwa katika kikosi cha wakubwa cha timu
ya taifa ya ujerumani.
Katika klabu yake ya Bayern, Schweinsteiger
alisaini mkataba julai 1998 akichezea timu ya vijana na kushinda taji la kombe
la vijana kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2002.
Baada ya kupata mafanikio hayo nyota
huyo alipandishwa kikosi cha wakubwa cha Bayern na kuwa miongoni mwa wachezaji
wa akiba.
Schweinsteiger alianza kucheza kama
winga wa kushoto na baada ya kocha Ottmar Hitzfeld kumwona katika mazoezi
alimwingiza dakika za mwisho katika mechi ya UEFA dhidi ya RC Lens mwaka 2002
na kupiga pasi ya mwisho iliyozaa bao muhimu la Markus Feulner.
Mwezi mmoja baadaye alisaini rasmi mkataba
na Bayern na kucheza mechi 14 za ligi kuu nchini Ujerumani katika msimu wa
2002-03 na kuipa klabu yake ubingwa.
Msimu uliofuata alicheza mechi 26 na
kufunga bao lake la kwanza katika mchezo dhidi ya VfL Wolfburg mwezi septemba
2003.
Akiwashangaza wengi kocha mpya wa
Bayern, Felix Magath mwanzoni mwa msimu wa 2005-06 licha ya uwezo wake
alimwondoa kikosi cha kwanza, lakini baadaye alirejeshwa katika mechi ya kwanza
ya robo fainali ya UEFA dhidi ya Chelsea na kufunga bao.
Ndani ya misimu mitatu hadi kufikia
mwaka 2007-08, nyota huyo alikuwa ameshacheza mechi 135 katika mashindano
mbalimbali ambayo Bayern ilishiriki na kufunga mabo 10.
April 2012, Schweinsteiger aliifungia
klabu yake penati ya mwisho na kuitupa nje Real Madrid kuwania kucheza fainali
ya UEFA na Bayern Munich kukutana na wazee wa Roberto Di Matteo kwa wakati ule,
Chelsea ambao waliwashinda Bayern kwa mikwaju ya penati katika uwanja wao wa
Allianz Arena na kutwaa ndoo ya UEFA.
Msimu huu wa 2012–13 UEFA mchezaji huyo mwenye kipaji kikubwa cha soka
anaendelea kufanya vizuri na kumiliki nafasi yake mbele ya nyota mpya Javi
Martinez.
Mbali na klabu yake Byern Munich, fundi
huyo mkubwa wa soka amepata mafanikio makubwa timu ya taifa ya Ujerumani.
Kufikia Octoba mwaka 2012,
Schweinsteiger alikuwa ameichezea timu yake ya taifa mechi 97 na kufunga mabao
23 tangu ajiunge nayo mwaka 2004.
Ameshiriki mashindano makubwa matano na
timu ya taifa, 2004, alicheza kombe la
mataifa ya ulaya nchini Ureno, 2006
kombe la dunia nchini kwao, 2008 kombe la mataifa ya ulaya Austria-Switzerland,
2010 kombe la dunia afrika kusini na 2012 kombe la mataifa ya ulaya nchini
Ukraine na Poland.
Pia alikuwemo katika fainali za
kihistoria za kombe la dunia baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi
ya Afrika yaani nchini Afrika kusini mwaka 2010.
Katika fainali hizo, Schweinsteiger aliitwa
kuziba pengo la kiungo wa kati, Michael Ballack aliyekuwa majeruhi na kuceza
kwa kiwango cha juu sana.
Alikuwa muhimu sana katika safu ya
ulinzi na ushambuliaji ya Ujeruman baadaye kutajwa kama mchezaji bora wa
mechi katika mchezo wa robo fainali
dhidi ya Argentina huku akitoa msaada wa pasi mbili zilizozaa mabao mawili kati
ya manne waliyoshinda mbele ya vijana wa Diego Armando Maradona mkwe wa
mchezaji wa Manchester city ya England, Sregio Kun Aguero.
Kwa bahati mbaya Ujerumani walipoteza
mchezo wa nusu fainali mbele ya mabingwa watetezi Hispania lakini walitwaa
nafasi ya tatu baada ya kuwabamiza Uruguay huku nyota huyo akiwa kama nahodha
baada ya nahodha Philipp Lahm kukaa benchi kutokana na maradhi.
Kwa ujumla katika fainali hizo za mwaka
2010 zilizofanyika nchini afrika kusini ,Schweinsteiger alisaidia mabao matatu
katika mechi saba na kwa kutambua kiwango chake, FIFA walimtunuku nyota huyo
tuzo ya kiatu cha dhahabu kinachotolewa kwa mchezaji aneyecheza kwa kiwango
kizuri muda wote wa mashindano.
Pia Katika mechi za kuwania kucheza
fainali za mataifa barani ulaya mwaka jana, ujerumani wakiwa kundi A, Nyota
huyo alijiimarisha zaidi kama kiungo wa ulinzi na kuisadia timu yake ya taifa kushinda
mechi kumi na kusaidia kufunga bao moja na kusaidia bao moja.
Kama ilivyo kwa binadamu yeyote, mbali
ya kazi yake kuwa soka, nyota huyo pia ana maisha yake nje ya uwanja ambayo
jamii inayatambua.
Schweinsteiger
anaishi na mpenzi wake Sarah
Brandner mjini Munich. Wawili hao wanapendana sana na mara nyingi wakati
nyota huyo hana majukumu katika klabu yake ya Bayern Munich anatumia muda wake
kukaa na mpenzi wake wakibadilishana mawazo kuhusiana na maisha yao.
Pia nyota huyo anasifika kwa ukarimu
wake na msaada kwa rafiki zake pale wanapopata shida na ndio maana ana
mashabiki wengi sana ambao wanamtania kwa jina la utani la "Schweini"
au "Basti" ili kumtofautisha yeye na kaka yake mkubwa Tobias ambaye
pia alichezea klabu ya Bayern.
Nyota huyo licha ya kufagilia mapenzi
lakini muda mwingi huutumia katika mazoezi ya timu na ya kwake binafsi na ndio
maana muda wote yupo kwenye kiwango cha juu akijihakikishia namba katika kikosi
cha kwanza cha Bayern Munich pamoja na timu ya taifa ya Ujerumani.
Mchezaji huyo mwenye nidhamu ya soka ni
mfano mkubwa wa kuigwa kwa wachezaji wa kitanzania ambao wengi wao hawajali
mazoezi ya timu na mazoezi bainafsi huku wakijiingiza kwenye starehe za
mapenzi, pombe na kuporomoka viwango vyao.
Uwezo wa “Bast” wa kupiga chenga,
kumiliki mpira, kucheza nafasi tofauti na kupiga mashuti ya uhakika na pasi za
mwisho ndio unaombeba mpaka sasa na atabaki kuwa moja kati ya wachezaji
wachache wenye vipaji vikubwa vya soka kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka
wa sasa.
0 comments:
Post a Comment