Na Baraka Mpenja
Kocha mkuu wa mabingwa wa zamani wa kandanda nchini Tanzania mwaka 1986 , klabu ya Tukuyu stars “Banyambala”, na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya vijana ya mkoa wa mbeya iliyoshiriki Copa Coca Cola 2011, Chuma Edson Amos amesema kupotea kwa klabu hiyo katika soka la ushindani nchini Tanzania kumechangia kushuka kwa soka la mkoa wa Mbeya.
Akizungumza na mtandao
huu, Chuma aliyewaongoza “Banyambala” na viatu vyao miaka ya 2011-2004 kabla ya
kushuka daraja alisema, klabu hiyo ilikuwa kitalu cha kuzalisha wachezaji
vijana hivyo kupotea kwake kumeligharimu soka la mkoa huo hasa maafande wa kupiga gwaride Tanzania Prisons
wanaowakilisha mkoa wa Mbeya ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Chuma alisema kihistoria
wachezaji wengi waliotamba na Prisons ya
ukweli wakiwemo Geofrey Bony, Shadrack John Nsajigwa, Ivo Mapunda na wengine wengi,
chimbuka lao lilikuwa Tukuyu stars ambayo kwa sasa inajivutavuta kurejea soka
la ushindani kufuatia mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela kuanzsisha mpango
wa kuifufua timu hiyo mwaka jana.
“Unajua Tukuyu stars
tulipika vijana wengi sana kutoka ndani ya jiji la mbeya, tulikuwa tunachukua
wachezaji wachache kutoka mikoa jirani ya Iringa, Ruvuma na Rukwa, lakini
tuliangalia zaidi nyumbani, na ndio maana tulifanikiwa kupata vijana wengi
wenye vipaji wakitawaliwa na nidhamu
kubwa ya soka”. Alisema Chuma.
Chuma alilisisitiza kuwa
kitendo cha viongozi wa timu ya Prisons na chama cha soka mkoani Mbeya
kushindwa kuwekeza kwenye soka la vijana kwa kuanzisha mashindano mbalimbali
baada ya michuano ya kitaifa ya Copa Coca Cola ndio chimbuko la timu hiyo
kuhangaika huku na kule iking`ang`ana kukwepa rungu la kushuka daraja msimu
huu.
“Vijana wakitoka Coca Cola
wanaachwa kama yatima, badala ya kuwaendeleza kwa pamoja ili waimarike zaidi
kimichezo wanatupwa tu, mfumo huu umeliweka rehani soka la Mbeya tofauti na
miaka ya nyuma”. Alisisitiza Chuma.
Mbali na kuongelea soka la
vijana jijini Mbeya, pia alitupia jicho la tatu soka la vijana la Tanzania na
mfumo wake.
BAADHI YA WACHEZAJI WA ZAMANI WA TUKUYU STARS KWENYE TAMASHA LA UZINDUZI WA KUIFUFUA TIMU HIYO |
Kocha huyo aliwataka viongozi wa shirikisho la soka Tanzania TFF kuacha
kasumba ya kujaza vijana wa mikoa mikubwa hasa Dar es salaam kwenye timu za
taifa za Tanzania.
Chuma aliongeza kuwa
wachezaji wengi wanaotamba katika soka la Tanzania kama Juma Kaseja, Jerryson
Tegete na wengineo, asili yao ni mikoani, kitu ambacho kinamaanisha vipaji vipo
zaidi ya Dar es salaam.
“Nakumbuka Serengeti Boys
iliweka kambi jijini Mbeya kwa muda wa wiki mbili, ilicheza mechi za kirafiki,
lakini cha kushangaza viongozi wa timu hawakuona hata mchezaji yeyote wakuongezwa kikosini siku za usoni, hakika ni
jambo la ajabu sana”. Alisema Chuma.
Aidha kocha huyo aliwata
viongozi wa soka kusoma alama za wakati kwani dunia nzima sasa inawekeza katika
soka la vijana.
Alisema ni wakati wa
kujenga vituo vya soka maeneo mbalimbali hasa mikoani pamoja na kuwaendeleza
vijana kwa kuanzisha mashindano mbalimbali mikoani na kitaifa.
0 comments:
Post a Comment