Tiketi kwa ajili ya pambano la
kimataifa la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Cameroon
(Indomitable Lions) zinaanza kuuzwa kesho (Febaruari 5 mwaka huu) katika
vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Viingilio katika pambano hilo
litakalochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kuanzia saa 11 jioni ni sh. 5,000 (viti vya kijani), sh. 7,000
(viti vya bluu), sh. 10,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 VIP
C, sh. 20,000 VIP B na sh. 30,000 VIP A.
Vituo vitakavyouzwa tiketi hizo
kuanzia saa 2 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni
Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Oilcom Ubungo,
Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni.
Vilevile tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi, na milango itafunguliwa saa 8 kamili mchana.
Wakati huo huo, kundi la kwanza
na la pili la wachezaji wa Cameroon tayari limetua jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya mechi dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa
keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Cameroon chini ya Kocha Jean Paul
Akono itafanya mazoezi kesho saa 11 jioni Uwanja wa Taifa. Nayo Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager yenyewe itafanya
mazoezi Uwanja wa Taifa leo saa 11 jioni.
12,984 WASHUHUDIA SIMBA, JKT RUVU ZIKITOKA SARE
Watazamaji 12,984 walikata tiketi
kushuhudia mechi ya namba 99 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana
(Februari 3 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa
sare ya bao 1-1.
Viingilio katika mechi hiyo
vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo jumla ya
sh. 73,532,000 zilipatikana. Kila klabu ilipata mgawo wa sh.
17,443,752.45 ambapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
11,216,745.76.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 8,869,704.64, tiketi sh. 3,183,890, gharama za
mechi sh. 5,321,822.78, Kamati ya Ligi sh. 5,321,822.78, Mfuko wa
Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,660,911.39 na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,069,597.75.
UCHAGUZI FRAT SASA KUFANYIKA FEB 14
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha
Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) uliokwama kufanyika mara
mbili, sasa utafanyika Februari 14 mwaka huu mjini Morogoro.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa FRAT
wanatakiwa kufika Morogoro siku moja kabla ya tarehe ya uchaguzi. Pia
wapiga kura na wagombea wanatakiwa kulipia ada za uanachama kwa mwaka
2013 kabla ya uchaguzi.
Wagombea ni Army Sentimea na Said
Nassoro (uenyekiti) wakati wanaoomba nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni
Juma Chaponda, Juma Mpuya na Tifika Kambimtoni.
Abdallah Mitole, Charles Ndagala
na Hamis Kisiwa wanawania ukatibu mkuu, nafasi ya Mhazini inagombewa na
Jovin Ndimbo. Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ni Kamwaga Tambwe wakati nafasi ya uwakilishi wanawake
yupo Isabela Kapera.
Wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Emmanuel Chaula na Samson Mkotya.
0 comments:
Post a Comment