Ndugu Walid Amani Kaburu, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa
wa Kigoma;
Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bara;
Mwenyekiti wa CNDD;
Katibu Mkuu
wa PPRD;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa mliopo;
Ndugu Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu
ya Taifa;
Watendaji Wakuu wa Serikali na Viongozi wa CCM wa
ngazi mbalimbali;
Wanachama wenzangu wa CCM;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote niruhusuni nianze kwa kuwashukuru viongozi, wana-CCM na wakazi
wa Kigoma kwa mapokezi
mazuri sana mliyonipa mimi na mke wangu Salma
MNEC wa Lindi Mjini tangu tulipowasili
mkoani hapa. Nawapongeza kwa kukubali kuwa wenyeji wa Sherehe za Kuadhimisha Miaka
36 ya Kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Lakini pongezi kubwa kwa kuandaa sherehe hii
kwa mafanikio makubwa. Utaratibu mpya wa
Katibu Mkuu na Wajumbe wa Sekretariet kutembelea matawi, kuzungumza na
wanachama na wananchi ni wa aina yake.
Ni mzuri na unafaa kuigwa.
Ni jambo la faraja na kujivunia kwamba
tunasherehekea Chama chetu kufikisha umri wa miaka 36 wakati kikiwa imara na
nguvu za kutosha za kupambana na kushinda katika mfumo wa vyama vingi uliodumu
kwa miongo miwili. Pia kwamba, nchi yetu
na watu wake bado ni wamoja, na kuna amani na utulivu licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo na kubwa
zinazotishia umoja na mshikamano wetu.
Ni jambo la kufurahisha na kutia moyo kwamba tunasherehekea miaka 36 ya Uhai
wa CCM wakati nchi ya Tanzania ikiendelea kupiga hatua kwa kasi katika
kujiletea maendeleo. Tena maendeleo
yaliyo dhahiri na yanayoonekana na wote isipokuwa, labda, wale ambao hutembea wakiwa
wamefumba macho.
Wana CCM wenzangu;
Uimara wa
Chama cha Mapinduzi na maendeleo yanayopatikana nchini chini ya uongozi wake ni
uthibitisho wa ubora wa sera zake na umakini wa viongozi wa CCM kuongoza Chama na kusimamia serikali katika
kutekeleza Sera na hasa Ilani za Chama cha Mapinduzi. Wana-CCM wenzangu tunayo kila sababu ya
kujipongeza na kutembea kifua mbele kwa mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa na yale
yanayoendelea kupatikana ndani ya Chama na katika taifa. Wananchi wa Tanzania nao hawana budi
kujipongeza kwa uamuzi wao wa busara wa kukiamini Chama cha Mapinduzi kiendelee
kuongoza nchi yetu. Nawaomba waendelee
na imani hiyo hiyo kwa miaka mingi ijayo. Mimi nawaahidi kwa niaba ya Chama cha
Mapinduzi, tena kwa kujiamini kuwa hatutawaangusha.
Ndugu zangu, Wana-CCM wenzangu;
Tuendelee kwa ari zaidi na nguvu zaidi kujenga na
kuimarisha Chama chetu. Hayo ndiyo maagizo ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM
uliofanyika tarehe 11 mpaka 13 Novemba, 2012 kule Kizota, Dodoma. Hayo ni
maagizo kwa Chama chenyewe na kwa Jumuiya zake.
Maagizo ya kujijenga na kujiimarisha yameainishwa vizuri katika Maazimio
ya Mkutano Mkuu wa Taifa uliopita.
Lakini, hii si mara ya kwanza ni maagizo ya Mikutano Mikuu yote
iliyopita, ya mradi wa Kuimarisha Chama III na ya Mageuzi ya Ndani ya Chama
yaliyoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa katika Kikao chake cha Aprili, 2011.
Maombi yangu kwa viongozi na wanachama wenzangu wa
CCM kote nchini ni kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa ukamilifu maagizo hayo.
Kwanza tuyasome na kuyaelewa vizuri na kupanga mipango na programu nzuri za
utekelezaji wake. Viongozi wa Chama tunao wajibu maalum wa kuwaongoza viongozi
walio chini yetu na wanachama wote katika kuelewa na kutekeleza Maazimio ya
Mkutano Mkuu wa Taifa uliopita, Mradi wa
Kuimarisha Chama na Mageuzi ya Ndani ya Chama.
Ndugu zangu;
Tunayotakiwa kufanya si mageni. Ni mambo
tunayoyajua na tumekuwa tunayafanya lakini tunakumbushwa na kusisitiziwa kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anayafanya,
tena kwa ufanisi wa hali ya juu. Chama
ni wanachama. Hivyo basi lililo la awali kabisa ni kutambua kuwa lazima
tuendelee kuongeza wanachama. Wanachama ndiyo Jeshi letu la kutuletea
ushindi. Ndizo kura zetu za uhakika za
kuanzia. Hivi sasa kitaifa CCM ina wanachama 6,042,791. Hizi ni kura nyingi kwa kuanzia. Tujitahidi tufikishe wanachama milioni 8 mpaka 10 mwaka 2015. Hakuna wa kutushinda. Hivyo basi ni muhimu
kuwa na wanachama wengi wenye imani ya dhati kwa Chama chao. Wanachama wenye ufahamu
mzuri wa Sera za Chama na Serikali yake, wasiokuwa na ajizi katika kutekeleza Sera
na maagizo ya CCM na walio tayari kukisemea na kukitetea Chama cha
Mapinduzi. Kuwa na viongozi na wanachama
ambao imani yao kwa Chama ni nusu nusu au uelewa wao wa mambo ni mdogo na si
makini katika kutekeleza wajibu wao ni jambo la hatari.
Kwa sababu hiyo viongozi wenzangu na wanachama
wenzangu hatuna budi kuongeza wanachama na kuhakikisha kuwa tunawatayarisha
vizuri kuelewa vyema Sera za Chama na wajibu wao kwa Chama chao. Lazima tujipange vyema kuzitekeleza na
kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wake. Suala la elimu kwa wanachama wetu na
kujipangia majukumu ya kufanya ndani ya Chama na katika jamii lilisisitizwa sana
katika Mkutano Mkuu wa Taifa uliopita na katika mradi wa kuimarisha Chama na
malengo ya mageuzi ya ndani ya Chama. Haya shime tutekeleze.
Viongozi kutembelea wanachama wetu na kuzungumza
nao, kuwaelimisha na kufafanua mambo mbalimbali ya Chama na Serikali na
kuwaelekeza wajibu wao ni jambo la lazima kufanya. Hali kadhalika, viongozi
lazima tuwatembelee wananchi kufafanua Sera za Chama chetu na masuala yahusuyo
nchi yetu na serikali. Pia tuwasikilize
mambo wanayotaka kupatiwa ufumbuzi au ufafanuzi. Yale mambo tunayoyaweza tuyajibu na yale tusiyoyaweza
tuondoke nayo tukayatafutie majibu kisha tuwape taarifa. Ni kwa kufanya hivyo tu Chama chetu kitajijengea
uhalali wa kuendelea kuongoza taifa kwani watu watatuamini na kutupenda. Tusipowatembelea wananchi na kuzungumza nao
tunaacha ombwe linalojazwa na wale wasiokitakia mema Chama cha Mapinduzi. Watu
wanaopotosha wananchi na kupandikiza chuki dhidi ya Chama chetu na serikali
yake. Wengine wanaweza hata kuchukua
sifa zetu isivyostahili na kujifanya ni wao waliofanya au kusababisha yawepo.
Hali kadhalika tuhakikishe kuwa vikao vinafanyika
ili viongozi wapate fursa ya kuzungumza mambo yahusuyo ujenzi wa Chama chao na
kupanga mikakati na mbinu za kutekeleza wajibu wao. Miongoni mwa mambo ambayo Chama chetu lazima kiyape kipaumbele cha juu ni pamoja na
kujenga uwezo wa kujitegemea katika kila ngazi.
Jambo hili tumelisemea kwa muda mrefu lakini hakuna kitu cha maana
kinachoonekana kufanyika. Wakati umefika
wa kulipa uzito unaostahili suala la
kujitegemea. Tusilipuuze jambo hili muhimu kwa uhai wa Chama chetu vinginevyo
mambo mengi yatatushinda kufanya na Chama kitadorora na kudhoofika.
Wapo baadhi ya wenzetu wamefanikiwa katika hili
ndani ya Chama na Jumuiya. Tuwatambue na
kuwasiliana nao ili watupe maarifa ya kufanya hivyo. Jambo hili si la hiari tena. Ni lazima
tuhakikishe tunaulizana katika kila kikao.
Viongozi wenzangu na Wana-CCM wenzangu;
Miongoni
mwa maagizo na maelekezo makuu na ya msingi sana ya Mkutano Mkuu wa Taifa ni
Umoja wa Chama chetu. Mkutano Mkuu wa
Taifa umetutaka viongozi tuwe wamoja, wanachama tuwe wamoja na viongozi na wanachama
hali kadhalika. Tushikamane kwa pamoja
kujenga Chama chetu kueneza sera, kutekeleza sera na kukipigania Chama
chetu. Ndiyo maana kauli mbiu ya Chama
chetu iliyotoka katika mkutano ule ilikuwa Umoja
ni Ushindi. Ndiyo Kauli Mbiu ya
maadhimisho haya ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM na ndiyo Kauli Mbiu mpaka
itakapotengenezwa nyingine.
Umuhimu wa umoja hauhitaji kuelezwa kwa muda
mrefu. Sote tunaijua misemo ya wahenga
isemayo Umoja ni Nguvu, Utengano ni
Udhaifu au Nguvu ya Mnyonge ni Umoja na kadhalika. Umoja ndiyo uliowawezesha wazee wetu kuongoza
harakati za kudai uhuru wa nchi yetu na kushinda. Kina Saadani, Abdul Kandoro, Alhaji Tawakal
Karago na wenzao wengi hawakuwa na nguvu za fedha wala silaha bali umoja wao
ndiyo uliyoiletea nchi yetu uhuru.
Wakati mwingine husononeka sana
ninapoona viongozi na wana-CCM wakifanya vitendo vinavyovuruga umoja na
mshikamano ndani ya Chama. Nawaomba
wenzangu tulinde umoja wa ndani ya Chama cha Mapinduzi kama mboni ya macho
yetu. Tukiwa na umoja wana-CCM
tutapendana, tutazungumza lugha moja, tutashirikiana vyema kupigania Chama
chetu na kuwapigania wagombea wa Chama chetu kwenye chaguzi za dola.
Pasipokuwa na umoja yote hayo hayawezekani. Na ninyi wa Kigoma mnajua ukweli wa athari
zake. Tumepoteza majimbo matano kwa
sababu ya mifarakano ndani ya Chama
chetu. Tunataka kuyakomboa majimbo yetu. Tutafanya hivyo tu iwapo tutakuwa wamoja na
tuna mshikamano ndani ya Chama chetu.
Tunataka kuyakomboa majimbo yetu.
Tutafanya hivyo tu iwapo tutakuwa wamoja na tuna mshikamano wa
dhati. Ni imani yangu kuwa sherehe hizi
na kazi nzuri aliyofanya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, Naibu Katibu Mkuu,
Mwigulu Nchemba, Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dkt. Asha-Rose Migiro na
Katibu wa Uenezi Nape Moses Nnauye itakuwa chachu itakayotufikisha katika
matumaini yetu hayo.
Ndugu
Viongozi na Wana-CCM wenzangu;
Jambo
lingine muhimu sana ambalo hatuna budi
kulisimamia kwa ufanisi mkubwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, ahadi za
Chama chetu na wagombea wetu wakati wa
uchaguzi na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi. Lazima tukumbuke kuwa Ilani ya Uchaguzi ndiyo
mkataba rasmi baina ya wananchi wa Tanzania na Chama cha Mapinduzi
walipotuchagua mwaka 2010 tuendelee kuongoza nchi yetu.
Ilani
ya Uchaguzi hujumuisha mambo ambayo tumewaahidi
Watanzania tutayafanya.
Wakatuamini wakatuchagua. Ahadi
ni deni, lazima tulipe. Lakini pia zipo
ahadi za papo kwa papo nilizotoa mimi, alizotoa mgombea mwenza, walizotoa
wagombea wetu wa ngazi mbalimbali na viongozi wa Chama wa ngazi
mbalimbali. Hizo nazo lazima tuzitimize.
Jambo lililo muhimu ni kuzitambua ahadi hizo na kuzitengenezea mipango ya
kuzitekeleza. Mimi hufurahi sana
viongozi na wananchi wanaponikumbusha ahadi za papo kwa papo tulizotoa ili tuzitekeleze.
Wana-CCM wenzangu;
Napenda
kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini tunaitekeleza vyema Ilani ya
Uchaguzi mliyonikabidhi mimi na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Ghalib Bilal na
Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kuinadi na baada ya ushindi
kuitekeleza. Nawaahidi kuwa hatutawaangusha
katika hilo kwani hatupendi kusutwa na wala hatupendi Chama chetu tunachokipenda
sana kinyooshewe kidole au kilaumiwe kwa kutokutimiza ahadi.
Tunaendelea kwa mafanikio makubwa kutekeleza mambo
tuliyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi. Tumepanua sana fursa ya elimu katika
ngazi zote kuanzia ya msingi, sekondari, ufundi stadi na vyuo vikuu. Tuelekeze
nguvu zetu katika kuimarisha ubora wa elimu kwa maana tumeongeza vyuo vya ualimu na idadi ya wahitimu ili kukabili upungufu
wa walimu nchini. Tunaendelea kuongeza maabara, vifaa vya kufundishia na vitabu
ili kuboresha elimu inayotolewa. Vilevile tunaendelea kusogeza kwa wananchi
huduma ya afya kwa kuongeza idadi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Tumeanza kuona dalili njema kwani vifo vya watoto na wajawazito imeanza
kupungua. Hivi sasa juhudi kubwa zinafanyika kudhibiti magonjwa yanayoua watu
wengi kama vile Malaria na UKIMWI.
Sambamba na juhudi hizo, tunaendelea kuboresha
miundombinu na upatikanaji wa umeme, maji na huduma nyingine za jamii.
Tunaelekea kufikia lengo letu la barabara kuu zote kuwa za lami na kuunganisha
mikoa yote kwa barabara za lami. Ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 11, 154 kwa kiwango cha lami
na madaraja makubwa na madogo unaendelea katika sehemu mbalimbali hapa nchini.
Ninyi wa Kigoma ni mashahidi wa kazi hiyo. Barabara ya Kigoma – Kidahwe - Uvinza
inaendelea kujengwa. Daraja la Mto
Malagarasi, ujenzi wake unakwenda vizuri.
Na kwa upande wa Tabora nako ujenzi wa barabara za lami umeanza mambo
ambayo yanaihakikishia Kigoma barabara nzuri kutokea Pwani. Hatujaisahau barabara ya Kidahwa-Nyakanazi. Tunaendelea kutafuta fedha kutoka kwa marafiki
lakini wenyewe tutaanza kidogo kidogo mwaka huu kuelekea Kasulu. Hapa mjini tutaendelea kuongeza barabara za
lami. Nafahamu kuwa ujenzi wa barabara Gungu-Airport,
Job Lusinde na Mji Mwema umechelewa.
Nimehakikishiwa kuwa kasi
itaongezeka. Pia tutaijenga kwa kiwango
cha lami barabara ya Gungu-Tibirizi.
Ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege
unaendelea katika mikoa mbalimbali. Kiwanja cha Songwa kimekamilika na kesho nitaweka
jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma.
Ndugu Wananchi;
Kama alivyoeleza Waziri Harrison Mwakyembe mipango
yetu haiishii hapa. Tutaendelea kukipanua
kiwanja hiki hadi kifikie kilometa 3
ili ziweze kutua ndege kubwa zaidi. Narudia kusema nia yangu ya kuona siku moja
Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kinakuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa nchi za
Maziwa Makuu. Inshallah heri. Safari za treni ya Reli ya Kati zimeanza na
tayari mipango ya kuagiza mabehewa mapya na vichwa vya treni vipya kutoka nje
inakamilishwa ili kuboresha huduma hiyo.
Kama mambo yataenda kama tunavyotarajia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu
hali ya usafiri itakuwa bora sana. Pia
tunaendelea kuboresha reli yenyewe na tuna mipango ya kujenga reli mpya pana
zaidi itakayofika mpaka Msongati, Burundi kutokea Uvinza.
Vile vile tumeendelea kuchukua hatua za kuongeza uzalishaji
na usambazaji wa umeme nchini.
Tunaendelea kutekeleza lengo la Ilani ya Chama chetu ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya Watanzania wawe
wamefikiwa na huduma ya umeme. Hivi sasa
tumefikia asilimia 18 kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Ninyi ndugu wa Kigoma mmenufaika na mpango
huu. Kigoma, Kasulu na Kibondo mmepata mitambo
mipya ya kuzalisha umeme. Mwaka huu tutaanza kujenga njia ya kusafirisha umeme
kutoka Kibondo kwenda Kakonko. Suala la
umeme kwa upande wa Uvinza nimelisikia nitawatuma wahusika wafuatilie ili umeme
upatikane saa 24 na kwa bei nafuu.
Nawaomba viongozi wa CCM muwe mstari wa mbele kuyasemea mafanikio
haya. Msiposema wapo wanaosema na
kuchukua sifa yetu wakabeba wao.
Ndugu wananchi;
Jana jioni nilipokea risala ya wazee wa Kigoma. Katika risala yao wazee wamenipongeza kwa
kasi ya maendeleo inayopata Mkoa wa
Kigoma katika nyanja mbalimbali.
Nawashukuru kwa maneno ya faraja inatupa moyo; kwani wapo wenzetu
wengine hapa nchini tumewafanyia mambo mengi lakini wagumu hata kusema asante. Wamebakia kulaumu kwa yale mapya
wanayoyataka, tena kwa lugha chafu. Wazee pia wameniomba nihamie Kigoma
nitakapostaafu, au nijenge nyumba ya kupumzikia hapa Kigoma. Nawashukuru kwa moyo wao wa upendo na ukarimu
nitafikiria ingawaje sijajua nani atanipa eneo la kujenga.
Ndugu wananchi;
Katika
risala yao wazee wameelezea pia kwamba hali ya upatikanaji wa maji bado haijatengemaa.Watu
wanapata maji kwa mgao na Mbunge akaongezea kuwa bei imepanda sana na watu
hutakiwa kulipa hata kama maji hawakupata inavyostahili. Nilimuita Mkurugenzi Mkuu wa KUWASA kutaka
maelezo na mipango ya kupata ufumbuzi.
Katika
maelezo yake Mkurugenzi wa KUWASA amekiri kuwepo kwa mgao wa maji na kupanda
kwa bei ya maji. Mgao upo kwa sababu ya
chanzo kilichopo sasa kuwa kidogo hivyo kuleta maji kidogo kuliko
mahitaji. Mahitaji ya maji kwa mji wa
Kigoma/Ujiji ni mita za ujazo 26,000 kiasi kinachopatikana sasa
ni mita za ujazo 15,000. Hivyo kuna upungufu wa mita za ujazo 11,000.
Lakini
Mkurugenzi alinipa habari njema kwamba upo mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia ikishirikiana na Wizara ya Maji
utakaomaliza tatizo hilo. Kitajengwa
chanzo kipya cha kutekea na kusafishia maji katika eneo la Amani. Upatikanaji wa maji utaongezeka na kufikia mita za ujazo 42,000 hivyo kuzidi mahitaji ya sasa kwa mita za ujazo 16,000 ambazo
zitatosheleza mahitaji ya mji wa Kigoma mpaka mwaka 2030. Yatajengwa matanki ya
kuhifadhi na kusambaza maji matano huko Mnarani, Chungu, Kigoma Sekondari,
Mlole na Mji Mwema. Pia mabomba
mapya makubwa ya urefu wa kilometa 70 yatatandazwa kote mjini na watu 10,000
kuunganishwa na kufungiwa mita. Kuhusu
bei ya maji alisema malalamiko yataisha pindi kila mtumiaji atakapofungiwa mita
na kulipa kadri anavyotumia. Heri sasa
wamewafikia asilimia 54 ya wateja na
mipango ya kuwafungia mita watumiaji waliosalia inaendelea.
Ndugu wananchi;
Wazee
wetu hao pia walilalamikia bei ya viwanja kuwa kubwa mno kwa mtu wa kawaida
kumudu, pembejeo za kilimo za ruzuku kutokutosheleza mahitaji na kuchelewa
kupatikana na mengineyo. Nimeahidi kuwa
mamlaka husika zitataarifiwa kuyatafutia ufumbuzi masuala hayo. Vile vile wazee
wa Kigoma walitahadharisha kuhusu kuwepo migogoro kidogo na kuhatarisha amani ya Mkoa na taifa kwa ujumla. Nakubaliana nao kwamba ni kweli ipo na
inaelekea kuibuka kila kukicha na ni kweli kwamba ni hatari kwa amani na
utulivu hapa nchini. Nimelisema jambo
hili mara baada ya Uchaguzi wa 2010 lakini wapo waliojaribu kunibeza na kudai kuwa
si kweli. Watanzania wenzangu haitasaidia kujifanya haipo wakati
ipo tunaiona na kuisikia. Nilisemea jambo
hili tena katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka kuomba viongozi wa dini
watusaidie. Kama wao watawakemea na
kuwakataza waumini wao, magazeti yao na radio zao zisilete mifarakano ya kidini
haitatokea. Niliwaomba wafufue utaratibu
mzuri wa mazungumzo baina ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu. Ulikuwa utaratibu wao si wa serikali. Ukitumika vizuri utatuepusha na mengi. Nawaomba waione haraka ya kufanya hivyo. Serikali itatimiza wajibu wake wa kulinda
amani kama hapana budi. Lakini, mzuie tusifikie hapo.
Ndugu wananchi;
Kabla
ya kumaliza napenda kuwasihi viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha
kushabikia siasa za kuigawa nchi yetu katika makundi ya dini, rangi, kabila na
mahali anapotoka mtu. Naomba tushabikie sera zinazojenga umoja na mshikamano
badala ya migawanyiko na mifarakano. Ni
siasa na sera ambazo hazina faida yeyote kwa nchi yetu na watu
wake. Ni siasa za maangamizi na mifano ipo mingi duniani na hata nchi jirani ya
kuthibitisha hayo. Inashangaza kuona baadhi ya wanasiasa wanafanya siasa za
chuki kuwa mtaji wao wa kisiasa. Nawaambia hawatafika popote. Nawaomba Watanzania
wenzangu msikubali kutumiwa na wanasiasa au mtu yoyote mwenye sera za aina hiyo. Wanaendeleza maslahi yao binafsi na siyo ya
taifa. Msikubali kuweka rehani maisha yenu na amani ya nchi yetu kwa ajili ya
maslahi ya mtu au kikundi fulani. Jiulizeni hivi, nchi hii ikichafuka mimi na
familia yangu tutaokolewa na nani?
Ndugu
viongozi na wanaCCM wenzangu;
Mwisho, napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza
sana wenyeji wetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Ndugu Kaburu, na
wale wote walioshiriki kuandaa sherehe hizi ambazo zimefana sana. Nawashukuru
pia wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki
matembezi ya mshikamano leo asubuhi na sasa katika kilele cha sherehe
hizi. Sina neno zuri la kushukuru zaidi
ya kusema asanteni sana.
Nawapongeza
tena viongozi, wanachama, makada, wapenzi na wakereketwa wa CCM kwa kutimiza
miaka 36 ya uhai wa CCM. Nawasihi tutoke
hapa tukiwa na ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ya kwenda kukijenga Chama
chetu kote nchini na kuwatumikia wananchi.
Daima tukumbuke Umoja ni Ushindi
na kwa pamoja tutashinda. Kidumu Chama Cha
Mapinduzi!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment