OFISI ZA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA, TFF |
WAGOMBEA TFF KUPATA FOMU KWENYE TOVUTI
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) inawaarifu wadau wote kuwa fomu za maombi ya uongozi wa TFF na
Tanzania Premier League Board (TPL Board) zinapatikana pia kwenye tovuti ya
TFF.
Wote wanaopenda kugombea uongozi katika vyombo hivyo
wanaarifiwa kuwa wanaweza kupata fomu hizo kwenye tovuti ya TFF (www.tff.or.tz) na wanatakiwa
kulipia fomu hizo katika akaunti ya TFF namba 01J1019956700 iliyoko CRDB tawi
la Holland House.
Fomu zikiambatanishwa na risiti ya malipo (receipt) au
malipo ya benki (deposit slip) zirejeshwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa mkono au
kwa barua pepe (email) ambayo ni [email protected] kabla ya
saa 10 kamili alasiri ya Januari 18 mwaka huu.
Kwa wagombea wanaorejesha fomu kwa mkono kuna fomu ya
orodha (register) ambayo wanatakiwa kusaini wakati wanakabidhi.
Kamati ya Uchaguzi
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA RUREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa
pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Januari 10 mwaka huu.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza
chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa RUREFA walivyo na imani
kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Rukwa.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya RUREFA chini ya uenyekiti wa Blassy Kiondo aliyeibuka mshindi
katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Sumbawanga.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Rukwa kwa kuzingatia
katiba ya RUREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA
na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa
mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Blassy
Kiondo (Mwenyekiti), Gregory Seko (Katibu), John Maholani (Mjumbe wa Mkutano
Mkuu TFF), Ayoub Nyaulingo (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Gloria Ndawa (Mweka
Hazina). Nafasi nyingine zitajazwa katika uchaguzi mdogo.
HONGERA KWA AZAM KUTWAA KOMBE LA MAPINDUZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa
pongezi kwa uongozi wa klabu ya Azam kwa timu yao kufanikiwa kutwaa Kombe la
Mapinduzi mwaka huu.
Kwa Azam kufanikiwa kutetea ubingwa huo inaonesha
jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kabla ya kuingia katika mashindano hayo ambapo
ilicheza fainali dhidi ya Tusker FC ya Kenya.
Pia ushindi huo utakuwa changamoto kwa timu nyingine
za Tanzania Bara zitakazopata fursa ya kushiriki michuano hiyo ya Kombe la
Mapinduzi mwakani. Michuano hiyo iko kwenye Kalenda ya Matukio ya TFF.
TENGA KUTOGOMBEA TENA URAIS TFF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amesema hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa
kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF
leo, Rais Tenga amesema wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda
ilikuwa na kuijenga TFF kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo
kutengeneza katiba na kanuni, jambo ambalo limefanyika.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga |
LEODIGAR TENGA, RAIS WA TFF |
“Wajumbe wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana.
Nilishafika pale pa kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi.
Na kazi hiyo tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,”
amesema Rais Tenga.
Amesema walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya
uamuzi, kuongeza wigo wa wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu
hakuwezi kutokea migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa kuidhibiti.
Rais Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF, kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa
TFF kwa hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha
uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.
Ametoa mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF,
kwani baada ya kujenga taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe
ikiwemo nini kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo mbalimbali.
“Tumeshatengeza mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya
kuendeleza mpira. Changamoto ni tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu
wengine wabebe hiyo ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,” amesema.
Pia amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na
wadau wa mpira wa miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari,
Serikali, klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa
mpira wa miguu nchini.
19 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TFF
Wadau 19 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za
uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Fomu hizo zimeanza kutolewa leo (Januari 14 mwaka huu)
ambapo wawili wamechukua nafasi ya Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba
ujumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.
Waliochukua fomu za umakamu wa rais ni Wallace Karia
na Ramadhan Nassib. Wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza
muda wake.
Waliochukua fomu za ujumbe ni Shaffih Dauda, Athuman
Kambi, Hussein Mwamba, Stewart Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona,
Vedastus Lufano, Twahili Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi,
Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James
Mhagama na Selemani Bandiho.
PONGEZI UONGOZI MPYA KATAVI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa
pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Katavi (KAREFA)
uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Januari 13 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza
chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KAREFA walivyo na imani
kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Katavi.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya KAREFA chini ya ukatibu wa Peter Hella aliyeibuka mshindi katika
uchaguzi huo uliofanyika ukumbi wa DC mjini Mpanda kwa kumshinda Emmanuel
Chaula kwa kura sita dhidi ya mbili.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Katavi kwa kuzingatia
katiba ya KAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KAREFA
na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa
mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa ni Hella (Katibu), Elias Mande
(Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Deo Bakuba (Mwakilishi wa Klabu TFF). Nafasi ya
Mwenyekiti haikuwa na mgombea wakati Mawazo Maso aliyekuwa mgombea pekee wa
nafasi ya Makamu Mwenyekiti alipata kura nyingi za hapana. Nafasi zilizo wazi
zitajazwa katika uchaguzi mdogo.
0 comments:
Post a Comment